Jumamosi 31 Januari 2026 - 21:13
Utambulisho na falsafa ya uwepo wa Hawza upo katika kuunganishwa kwa kina na Mahdawiyya

Hawza/ Ayatollah A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini Iran, huku akisisitiza kwamba utambulisho na falsafa ya uwepo wa Hawza ya Elimu ya Kiislamu upo katika muunganiko wa kina na Mahdawiyya (imani ya Imam Mahdi) na matarajio yenye uhai, alisema: Muunganiko huu wa msingi ndio unaoitofautisha Hawza ya Kishia na taasisi nyingine zote za kielimu na kidini duniani, na unaweka jukumu zito la kihistoria juu ya mabega ya wanafunzi na wasomi wa Hawza katika kuendeleza njia ya ujenzi wa ustaarabu wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini, katika hafla ya kufunga duru ya tisa ya mashindano ya kielimu ya Hawza, yaliyofanyika katika kituo cha Wasaidizi wa Mahdi (a.j) mjini Qom, alirejelea nafasi ya kihistoria na ya kistaarabu ya Hawza ya Qom na kusisitiza: utambulisho na falsafa ya uwepo wa Hawza ya Elimu ya Kiislamu upo katika muunganiko wa kina na Mahdawiyya na matarajio hai, na muunganiko huu ndio unaoitofautisha Hawza na vituo vingine vya kielimu na kidini duniani.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini, huku akiziadhimisha siku za mwezi wa Sha‘ban na tukiwa karibu na kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani, aliitaja miezi hii miwili kuwa ni “fursa adhimu isiyokuwa na mfano kwa safari ya kumkaribia Mwenyezi Mungu na maandalizi ya kuinuliwa kiroho,” na akaongeza: mwezi wa Sha‘ban ni jukwaa la kuelekea vilele vya kiroho, na Ramadhani ni mwezi wa kunufaika kikamilifu na wa ukuaji wa kipekee kwa wanafunzi na wanazuoni wa Hawza.

Kumbukumbu ya kufariki mwanzilishi wa Hawza ya Qom ni nukta muhimu katika historia ya Ushia

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini Iran, akiashiria kuambatana kwa hafla hii na kumbukumbu ya kufariki marehemu Ayatollah al-‘Udhma Haj Sheikh Abdulkarim Haeri Yazdi (r.a), mwanzilishi wa Hawza ya Qom, alinukuu sehemu za ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu “Hawza inayoongoza na iliyo mfano,” na kusema: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi alitaja kuanzishwa kwa Hawza ya Qom kuwa ni kuchomoza kwa nyota katika giza kuu zaidi la historia ya dini nchini Iran; wakati ambapo udikteta wa Reza Khan ulikuwa ukijaribu kwa nguvu zote kuifuta dini na taasisi ya wanazuoni wa Kiislamu.

Ayatollah A‘rafi aliongeza kuwa: umahiri mkubwa wa Ayatollah Haeri (r.a) ulikuwa ni kuasisi taasisi hai, yenye mwendo na yenye uwezo wa kujenga ustaarabu kwa jina la Hawza ya Elimu ya Kiislamu; taasisi ambayo licha ya mashinikizo makali, haikuendelea tu kuwepo bali kutoka ndani yake jua kama Imam Khomeini (r.a) lilichomoza na kubadilisha mwelekeo wa historia ya Iran na ulimwengu wa Kiislamu.

Akizungumza moja kwa moja na wanafunzi na wasomi walioshiriki mashindano ya kielimu, alisisitiza: Hawza ya Elimu ya Kiislamu leo ni amana kubwa iliyowekwa juu ya mabega yenu ninyi wajenzi wa kesho, na jukumu la kuendeleza njia hii ya kihistoria na ya kistaarabu, leo limeelekezwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa kizazi cha vijana na wasomi wa Hawza.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini Iran, alielezea nafasi ya Mahdawiyya na kwa kufafanua “nukta tano za mizizi ya Mahdawiyya,” alisema: mtazamo wa matumaini juu ya mustakabali wa binadamu una mizizi ya kimaumbile na ya kibinadamu, ambao umejitokeza katika dini mbalimbali, hasa dini za tauhidi, na kisha katika Uislamu kwa uwazi na kina zaidi.

Aliongeza kuwa: katika madhehebu ya Kishia, Mahdawiyya hufikia kilele cha udhihirisho wake, kwa sababu fikra hii si ahadi ya kihistoria tu, bali inategemea uwepo wa Imam Ma‘sum aliye hai na aliyopo, ambaye japokuwa yuko katika ghaiba, ana athari na uongozi katika ulimwengu wa kimaumbile na kisheria.

Ayatollah A‘rafi alisisitiza kwamba: Mahdawiyya katika fikra za Kishia ina ramani dhahiri ya mustakabali wa binadamu na ustaarabu wa mwisho wa mwanadamu, na muhimu zaidi imeunganishwa na dhana ya “kusubiri kwa uhai”; kusubiri ambako ni roho ya majukumu yote ya kidini na mwelekeo wa maisha ya mtu binafsi na ya kijamii ya waumini katika zama zote.

Utofauti wa Hawza ya Elimu ya Kiislamu na vituo vingine vya kielimu duniani

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu ya Kiislamu, huku akisema kuwa vituo vya kielimu na kidini duniani ni vingi, alibainisha kuwa: kinachoitofautisha Hawza ya Kishia na vituo vyote hivyo ni muunganiko wake wa kina na Mahdawiyya na matarajio. Falsafa ya masomo, utafiti, ufundishaji, tablighi na hata mashindano ya kielimu katika Hawza ni kuunganishwa na kitovu hiki cha uongofu na uongozi wa Mwenyezi Mungu.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini, akirejelea nafasi ya wasomi wa Hawza, alitahadharisha pia kuhusu hatari za kipaji na akasema: kipaji na uwezo, ikiwa haviambatani na juhudi, jihadi ya kielimu na utakaso wa maadili, vinaweza kugeuka kuwa maradhi kama kujiona bora, uvivu, pupa na kufanya kazi kwa uzembe.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu ya Kiislamu alisisitiza: kipaji hakiwezi kuchukua nafasi ya kazi na jitihada endelevu, na wanafunzi vijana wanapaswa kuzitumia kikamilifu zama za ujana kwa juhudi kubwa za kielimu na kiakili.

Mapinduzi ya Kiislamu: mjadala wa kistaarabu unaopinga mfumo wa fikra za Magharibi

Ayatollah A‘rafi alielezea Mapinduzi ya Kiislamu kuwa zaidi ya mabadiliko ya kisiasa, na akasema: Mapinduzi ya Kiislamu yamepinga misingi ya kifalsafa, kima‘rifa na ya kistaarabu duniani, na yamewasilisha fikra mpya mbele ya mantiki ya ustaarabu wa kisasa wa Magharibi; fikra ambayo leo, kutokana na uwezo wake wa kimataifa na wa kimaumbile, inakabiliwa na mashinikizo na uadui mkubwa.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu nchini Iran aliongeza: Mapinduzi ya Kiislamu yana uwezo wa kuteka maeneo ya fikra duniani, na uwezo huu ndio chanzo cha hofu ya madola ya kibeberu.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Kiislamu, huku akisisitiza misimamo ya wazi na ya pamoja ya Hawza ya Elimu ya Kiislamu, alisema: Hawza ya Kiislamu katika ngazi zote ipo pamoja na wananchi, ni mtetezi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ni msaidizi thabiti wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi; na mbele ya vitisho, mashinikizo na fitna, itasimama imara juu ya misingi ya Uislamu, demokrasia ya kidini na uhuru wa nchi.

Ayatollah A‘rafi, mwishoni alibainisha kuwa: taifa la Iran pamoja na vijana wake wako tayari kuilinda na kuitetea misingi ya kimungu na ya kimapinduzi, na maadui wafahamu kwamba taifa hili halitarudi nyuma kutoka katika misimamo yake ya haki na ya msingi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha